[ [ Declaration of Beliefs ] ]
 

Available Languages:

UTANGULIZI

Sisi, tulio wa ushirika wa Filadelfia na ukweli wa Yahweh, msingi wa imani yetu unatokana na maandishi matakatifu yaani Biblia. Tunatambua upendo kama nguzo ya imani yetu. Ahadi walioweka washiriki wenye kujitolea wa shirika hili ni amri mbili kuu kama alivyozinena mwokozi wetu katika Matayo 22:37-40. Yahshua akamwambia, 'mpende Yahweh Elohim wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena na ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi hutegemea torati na manabii. Fundisho hili la Yahshua latoka moja kwa moja kutoka torati. Amri la kwanza kuu yatoka Kumbukumbu la Torati 6:4-9 na la pili liko Mambo ya Walawii 19:18. Upendo ndio msingi halisi katika hizi amri mbili. Amri hizi mbili ndizo nguzo ya zile amri zote za magaano naYahweh. Upendo ulioelezwa hapa unaakisi kiini cha sheria nzima ya Yahweh. Yahweh amedhihirisha upendo wake kwa wanadamu kwa kupeana mwanaye (Yohana 3:16-21). Yahweh ni upendo (1 Yohana 4:7-8, 16). Upendo ni muhimu sana katika imani yetu kama wafuasi halisi wa Yahweh katika Yahshua (1 Wakorintho 13)

Azimio letu kama waumini wa agano jipya, ni kutimiza hizi amri mbili kuu kwa kuhakikisha sheria zaYahweh zimeandikwa katika akili na pia roho zetu (Yeremiah 31:31-33; Waebrania 8:8-11; Waebrania 10:16-18). Haya yatafanikishwa tu tukiwa Waisraeli na Wayahudi kiroho ambao wamepasawa tohara katika roho na mawazo ili tuenende kadiri ya sheria za agano za Yahweh (Warumi 2:28-29, Wagalatia 6:15-16). Twaamini wanaomiliki upendo wa kweli wa Yahweh kwa hiari yao wataziweka Amri za Yahweh iwe dhihirisho la huo upendo. (1 Yohana 5:1-3). Wanaomfahamu Yahshua hutimiza amri zake na kuenenda katika njia zake. (1 Yohana 2:3-6) Yahshua aliwatambua wafuasi wake halisi kwa ule upendo wa Filadelfia kati ya mmoja na mwingine (Yohana 13:34-35). Aliendelea kuhimiza wazi ya kwamba lazima tupendane (Yohana 15:12-13) na wale wenye mapenzi ya Yahshua watapeana maisha yao kwa wa wapendao.

Kutokana na kufahamu vizuri hasa upendo wa kweli wa Yahweh, ni azimio letu kuwa jinsi lile kusanyiko la Filadelfia lililokuwa (Ufunuo 3:7-13). Walio wa kusanyiko hili wametimiza neno la subira la Yahshua (amri za Yahweh) –Yohana 14:21-24) wala hawakukana jina lake. Kwa kule kujitolea kwao, Yahweh atawalinda, watoke katika saa ya kuharibiwa iloyo tayari kulijia ulimwengu wote mwisho wa nyakati (Ufunuo 3:10). Katika unabii, waumini wa kweli wa nyakati za mwisho ni wale walio shika ushuhuda na imani ya Yahshua na Amri za Yahweh. (Ufunuo 12:17 na 14:12) Hivyo twajitolea kufuata amri za Yahweh zile za agano hili kwa njia ya kupendana. Kuwa na upendo wa Filadelfia maana yake ni kuwapenda wandugu na wandanda na hata watu wote. Yahshua atuhimiza kuwapenda watu wote na hata maadui (Matayo 5:42-44). Hivyo twajitolea kuwapenda wote bila fikira ya jinsia, ukoo, imani, rangi, dini au hata Uraia. Nyumba ya kiroho ya Yahweh itaitwa Nyumba ya sala ya watu wote (IsaYa. 56:6-8)

Twaelewa nyakati hizi za mwisho Yahweh anawafanya walio wake kurudi kwake kwa njia ya kuzitunza amri zake. Kwa njia ile ile ya unabii kupitia nabii EliYah (Maana yake “Yahweh ndiye Elohim wa kweli), anawarudisha walio wake kwake kwa njia ya imani ya kweli (Malaki 4:4-6) Mwanaye, Yahshua Masihi, ndiye neno aliyefanyika mwili (Yohana 1:14) na ndiye ufunuo asili wa sheria timilifu zaYahweh, sheria ya uhuru, inayo okoa kabisa nafsi zetu. (Yakobo 1:21-25). Hivyo twafahamu shabaha yetu ya kudhihirisha upendo wa Yahweh, Yahshua, na hata mwanadamu mwenzetu kwa kutunza amri zake Yahweh. (1 Yohana 5:3, Yohana 14:15). Katika kutenda haya twadhihirisha mapenzi yetu kwa Yahweh na tutahesabiwa wakamilifu na welekevu mbele za Yahweh (Yakobo 2:14-26) Kama watu wa imani, tunawajibika kuonyesha imani yetu katika matendo yetu (na ndiyo kutunza sheria). Matendo yetu mema ndiyo yanaonyesha imani yetu. Hatukosi kufahamu tumekombolewa na neema wala si kwa matendo (Waefeso 2:8-10)

Wokovu ni zawadi Yahweh anapeana bure bali si kitu unafanyia kazi. Yahweh anawapea wote wanaoweka agano na yeye katika damu la agano lililotiririka ile tuokoke (Warumi 3:21-26) wakishikilia ile imani mpaka mwisho (Matayo 24:13)

Tumebainisha neno la Yahweh ndilo kweli (Amri Ya Agano) (Yohana 17:17) na ndiyo hutakasa na kufungua wote watoke katika minyororo ya dhabi (Yohana 8:31-36) na njia zake haribifu (Warumi 6:23). Uasi ama dhambi ni uvunjaji wa sheria (1 Yohana 3:4) Ujuzi wa dhambi wapatika tu katika kufahamu sheria za Yahweh (Warumi 7:7). Bila huo ufahamu, ni ngumu kutambua dhambi, na hivyo kutumbu au kumrudia Yahweh

Wanao mwabudu Yahweh sharti wafanye hivyo katika roho na katika kweli. (Yohana 4:23-24). Twajitolea kumiliki na kudumisha Roho Mtakatifu katika maisha yetu na katika mwili wa waumini kwa kuwa waaminifu kwa ukweli wa Amri za Agano la Yahweh. (Matendo 5:32)Twajitahidi kuwa watu wa Kiroho machoni mwa Yahweh kwa kuzaliwa mara ya pili katika ubatizo (Katika Jina la Yahshua Masihi) na roho mtakatifu (Roho Wa Yahweh) na hivyo kujiandaa kurithi ufalme wa Yahweh. Hii ni chanzo tu cha kubadilika kunaoanza mtu akiona haja ya kutumbu na kubadilika ndani yake na tena kubatizwa. Utaratibu huu wa kugeuzwa utafikia kilele chake tukigeuzwa tuwe mili ya kiroho Yahshua atakaporudi na ule Ufalme wake. (Yohana 3:3-7, I Wakorinto 15:35-54)

Tulio wa kusanyiko hili la Filadelphia na ukweli wa Yahweh tumeungana pamoja ili kufanya mapenzi ya Baba Yetu aliye Binguni, tukijipeana kwake kama mashahidi wake, na sote pamoja tukihubiri ule ukweli wa neno la Yahweh mpaka mwokozi Yahshua atakaporudi. Haya yakisha semwa kwa ufahamu kamili na kujitolea ndiyo tunatoa hii “Maadili Ya Imani” kama ushuhuda wa imani yetu katika Masihi Yahshua na kubainisha kanuni msingi hasa wa imani yetu katika mpango wa wokovu.

MAADILI HASA YA IMANI YETU

Sisi walio wa kusanyiko la Filadelphia na ukweli wa Yahweh, tunakubali imani ifuatayo jinsi ilivyo andikwa katika Neno La Yahweh, kama Yahweh alivyo tupea ufahamu kwa neema yake kupitia Roho Mtakatifu.

 1. Tunatangaza Muweza Yote, Yahweh ndiye Muumbaji Mukuu aliyeumba vitu vyote na niyeye tu anayestahili kuabudiwa kama Elohim wa kweli wa dunia. (Mwanzo 1 na Kutoka 20:2-6). Amejifunua kwa watu wake kwa jina moja na lililo kuu Yahweh (Kutoka 20:2 na 7;Mwanzo 12:8,26:25. kutoka 3:13-15). Jina Yahweh maana yake ni “Aishiye Milele.”Jina lake latokana na kitenzi cha Kiibrania cha Kuishi ama kudumu. Ni yeye tu anaweza kupeana uhai na vilevile hata kuuchukua (Ayub 1:21). Jina lake ni la muhimu sana kwa watu wake, wanalifahamu jina lake na wanaitwakwa hilo Jina Lake. (Yohana 17:6, 11-12; 2 Mambo ya Nyakati 7:14; Isaiah 52:6) Wale 144, 000 katika kitabu cha Ufunuo wana Majina ya Mwana na Baba yameandikwa katika mapaji ya nyuso zao (Ufunuo 14:1) Yahweh ni Roho na wale wamwabuduo imewapasa wafanye hivyo katika Roho na Kweli (Yohana 4; 23-24). Ili kumpendeza Yahweh lazima tuamini yeye yuko na kwamba atatupea thawabu tukiendelea kumtafuta kwa bidii (Waebrania 11:6) Mwishowe watu wa Yahweh watajumuika naye katika ile enzi ya mbingu mpya na nchi mpya (Ufunuo 21:1-8). Yahweh atashuka dunia hii na ataanza ule mji mtukufu tunao utaraji-Yerusalem Mpya (Ufunuo 21; 9-27). Atapea maji ya uzima na hata tunda la ule mti wa uzima wale walioandikwa jina lake katika mapaji ya nyuso zao. (Ufunuo 22:1-4). Yahweh atapea mwanga watu wake wakitawala pamoja naye katika ufalme wa milele. (Ufunuo 21:23 na 22:5)

 2. Tunatangaza Yahshua Masihi ndiye mwana wa Yahweh (Matayo, 3:16-17, Marko 1:9-11;Luka 3:21-22). Alikuja na mwili na akazaliwa na bikira. (Isaya 7:14;Matayo 1:23.)Akiwa mwokozi wa ulimwengu, alidhihirisha mapenzi ya Yahweh kwa wanadamu (Yohana 3:16-21). Maana ya Jina lake ni “Wokovu wa Yahweh”(Matayo, 1:21). Kabla ya kuja katika mwili, Yahshua alikuwa kiumbe cha Kiroho aliyeumbwa adumu milele (Ufunuo 3:14, Wakolosai 1:15;Yohana 17:5, Mithali 8:22-31). Ni yeye alikuwa neno katika kazi ya Yahweh ya kuumba na vitu vyote vilikuwa kwa ajili yake. (Wakolosai 1:16-17, Waebrania 1:1-2, Yohana 1:1-3, 10, Mwanzo 1). Ni kiumbe aliye tofauti walakini aliye mmoja katika kusudi na Yahweh (Yohana 10:30) kama vile bwana na bibi walio wawili lakini moja katika kusudi ya ndoa. (Mwanzo 2:24) Kupitia kwa umoja wa roho katika patanisho la imani (Waefeso. 4:1-7) anakusudia walio wake wawe mmoja wakishikana nayeye na hata Baba Wetu wa Mbinguni. (Yohana 17:21-22, Kumbukumbu la Torati, 6:4) Pamoja na Yahweh, Yahshua pia ni Elohim (Yohana 1:1). Aliishi maisha bila dhambi (I Petero, 2:22). Kama mwana-kondoo wa Yahweh, alikufa kwa dhambi za walimwengu (Mwanzo, 3:15, Isaya, 53:4-6, Yohana 1:29, 35 Warumi 3:24-26;Wagalatia 1:3-5, Waefeso 1:7,;5:1-2,;Wakolosai 1:20-22;Waebrania 9:12, 15, Ufunuo 5:9-10). Baada ya siku tatu, usiku na mchana, alifufuka toka kwa wafu (Matayo 12:36-40, Matayo 28:1-2). Kwa sasa yuko mbinguni katika mkono wa kulia wa Baba Yahweh (Matayo 22:44. Marko 16:19 Waebrania 1:3, 13:12:2). Yeye ndiye mpatanishi wa agano jipya katikati mwa Yahweh na watu wake (1 Timotheo 2:3-7, Waebrania 9:15:12:24.) Yahshua ndiye kichwa cha mwili wa wanao amini (Waefeso 4:15, Wakolosai 1:18). Mwishowe wa mambo yote ya ulimwengu, atarudi hapa duniani na kusanya walio wake katika kule kufufuka kwanza ili wakaingie Ufalme Wa Yahweh utakao kuwa hapa duniani (Matayo 24:29-31, 1 Wathesalonike 4:16-17, Ufunuo 19:11-16) Atatawala miaka elfu moja na wengine wa ufufuko wa pili watahukumiwa katika kile Kiti Cheupe Cha Enzi (Ufunuo 20, Yohana 5:22-29,). Nyumaye atamkabidhi Baba Mambo yote na Yahweh atakuwa pamoja na watu wake katika mbingu na nchi mpya. (1 Wakorintho 15:24-28, Ufunuo 21 na 22).

 3. Tunatangaza Roho Mtakatifu ni nguvu itokayo mbinguni. (Matendo Ya Mitume 1:8). Roho si kiumbe. Ni nguvu za Yahweh za kutenda kazi. Neno la Kiyahudi la Roho ni “ruach” maana yake ikiwa pumzi ama upepo. Katika Ugiriki hii nguvu yaitwa “pheuna”maana yake pepo inayofuma ama hewa (Matendo 2:1-4). Roho Mtakatifu ni pumzi ama Nguvu za Yahweh zinazoenenda kutimiza malengo yake. Yahshua aliahidi kutoa nguvu ya Roho Mtakatifu kwa mitume wake ili wakashuhudie ukweli wa wokovu ulimwenguni kote. (Matendo 1:8) Baba alimtuma Roho Mtakatifu kama mliwaza na kuleta ukumbusho wa mambo yote kwa jina la Yahshua. (Yohana 14:25-26). Wale walio na Roho Mtakatifu ndani yao hukumbuka amri za Yahweh na hutimiza amri za vishanda kiroho (Hesabu 15:37-41, Kumbukumbu La Torati 22:12) Roho Mtakatifu ndiye roho wa kweli (Yohana 14:16-17, 15:26-27, 1 Yohana 5:7) na hupeanwa tu kwa wale wanaotii agano la Yahweh katika Yahshua Masihi (Matendo 5:32). Wanaobatizwa katika jina la Yahshua Masihi hupokea kipawa cha Roho Mtakatifu kwa kuwekelewa mikono na Wazee (Matendo 2:38, 8:15-17, 19:6) na wanatiwa muhuri na yule Roho wa ahadi (Waefeso, 1:13-14). Inakuwa ni juu yao kutunza huyo Roho kwa kuzaa matunda yanayolingana na mapenzi ya Roho (Wagalatia 5:22-26) na pia karama za roho (1 Wakorintho 12:1-11). Ndiye Roho wa Uhai ambaye tunastahili kuenenda kwa njia zake (Wagalatia 5:16, 25). Yu adumu ndani ya wale wanaostahili kuitwa “Wana wa Elohim”. (Warumi 5:1-17). Twaamini yale mafunzo ya “utatu mtakatifu” hayatokani na maandishi na ilitokana na makafiri wasio mjua Yahweh.

 4. Tunatangaza wote wenye imani ya kweli ya Yahweh na Yahshua, imewapasa kuthibitisha imani yao kwa kutunza Amri za Agano ya Yahweh kutoka nyoyo zao (Waebrania 11). Isipokuwa zile dhabihu za kuchinja wanyama ambazo ziliisha Masihi wetu alipofanyika kondoo wa dhabihu kwa dhambi zetu (Mwanzo 3:15, 21 ;Zaburi 51:16-17), sheria za Yahweh zingali zinatumika (Matayo 5:17-20). Masihi alifundisha kama tutaingia katika ule uzima inatupasa kutunza amri (Matayo 19:17) Kwa kujichagulia Yahshua awe neno lilofanyika mwili kwa kutii Sheria za Agano ya Yahweh kwa kuonyesha mapenzi, tunajichagulia uzima (Kumbukumbu 30:15-20 , Yohana 1:12-14). Kwa kutii na kusifu, twatoa dhabihu za Kiroho kwa Yahweh kupitia kwa Yahshua Masihi (Hosea 14:2, Wafilipi 4:18, Warumi 12:1, Zaburi 107:22, Zaburi 116:17, 1 Petro 2:5) Twafahamu hata sheria zinazokisiwa ndogo na ni za Yahweh kuna haja zitunzwe (Matayo 5:17-20)

 5. Tunatangaza dhambi ni uvunjaji wa sheria za Yahweh (1 Yohana 3:4) Dhambi ndiyo inatutenganisha na Baba Yahweh (Isaya 59:1-8) Kwa dhabihu aliyotoa , Yahshua aliondoa lile kuta iliyotenganisha Yahweh na watu wake, akatufanya tukubalike, akatuhuisha kwa dhabihu na damu ya mwanawe (Waefeso 2, Isaya 53). Tunazo nguvu juu ya dhambi, kwa kukubali Yahshua awe mwokozi na mkombozi wa maisha yetu, Kwa kuenenda katika njia zake na kutii amri zake (Micah 6:6-8, I Yohana 1:5-10 na 2:1-6). Mshara wa dhambi zinazofanywa makusudi ni kifo (Waebrania 10:26-31)

 6. Tunatangaza msahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23) Mauti ya kwanza ni kule kufa kwa mwili huu na kutaendelea mpaka kufufuka mbali kuna mauti ya pili ambayo ni kuangamizwa kabisa katika ziwa la moto (Jehanamu) na imewekewa wale , sababu ya matendo yao maovu, majina yao hayako katika kitambu cha uzima (Ufunuo 20:11-15 na 21:8). Twaona yale mafunzo ya “roho asiyokufa” hayatokani na Bibilia (Ezekieli 18:4, 20, Ufunuo 20:14-15, Ufunuo 21:8). Huu ndiyo uongo wa kwanza , shetani akimndanganya Hawa katika bustani la Edeni “Mwanzo 3:3; Mtu anapokufa kimwili, hutokwa na pumzi ya uhai (kwa Kiyahudi—Neshamah) na hukaa katika hali ya kutojifahamu (usingizi) mpaka atakapofufuliwa (Mwanzo 2:7, Danieli 12:2, 1 Wathesalonike 4:13-17;Kohelethu 9:5). Yahshua pekee ndiye aliye paa mbinguni (Yohana 3:13, Matendo 2:34). Wote wataokosa nafasi katika kule kufufuka kwa kwanza watasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Yahshua Masihi baada ya utawala wa miaka elfu moja wahukumiwe kadiri ya matendo yao na ujuzi wa ukweli walio nao (Warumi 2:12-16, Ufunuo 20:12-13). Lile ziwa la moto ni moto uchomao ukileta mauti papo hapo, jinsi moto ulivyo choma Sodoma na Gomorah wala sio moto wa mateso milele (Yuda 1:7, Isaya 66:24, Malachi 4:1-3) Ibilisi Shetani ni kiumbe kilichoko na ndiye baba na mwanzilishi wa uongo, anayepinga ukweli (Yohana 8:44, Mwanzo 3:1-5,, Ayub 1:6 na 2:1) Yeye ndiye yule joka, mwenye kundanganya ulimwengu na kushtaki wandugu (Ufunuo 12:7-10) Lengo lake ni kudhuru na kuharibu kazi ya Yahweh na kuwatolea vita wanaoshishika na kuzitunza amri za Yahweh (Ufunuo 12:17) Katika utawala wa miaka Elfu Moja wa Yahshua, shetani atafungwa (Ufunuo 20:2-3). Baada ya hiyo miaka kuisha, atafunguliwa ili andanganye mataifa tena. Kisha ataangamizwa katika lile ziwa la moto (Ufunuo 20:7-10).

 7. Tunatangaza kutubu dhambi, kukifuatiwa na kubatizwa katika jina la Yahshua Masihi, ndio tendo kamili la kuweka agano na Yahweh (Matendo 2:38, Warumi 6). Ubatizo hufanyiwa mtu mara moja, akisimama atubukizwe kwa maji na nyuma, katika jina la Yahshua Masihi. Ni tendo takatifu linalosimamia kufa kwa matendo ya umwili, na ufufuo wa roho safi wa binadamu katika kufa na kufufuka kwa Yahshua Masihi (Warumi 6:4-11). Tendo hili ingawa lafanyiwa mwili laashiria ubadilko wa ndani utakaoleta hakikisho kwamba mtu ameacha matendo ya kimwili na kugeuka kuongozwa na Roho mtakatifu wa Yahweh (Wakolosai 3:1-17). Mwenye kubatizwa lazima awe ametimiya umri wa kuwajibika, karibu umri wa miaka 20,(tukizingatia pia uzima wa kiroho) ili afikiriwe kwa kubatizwa (Hesabu 1:2-3, 14:29 na 32:11) wale wamebatizwa katika jina la Yahshua Masihi na kudumu katika hilo agano watakuwa katika kule kufufuka kwa kwanza na kumlaki Yahshua mawinguni atakaporudi na ule ufalme wa Yahweh utakaokuwa hapa duniani (Matayo 24:29-31:1 Wathesalonike 4:13-17: 1 Wakorintho 15:50-58). Hawa waumini wenye kutii watatawala pamoja na Masihi katika huo ufalme hapa duniani (Ufunuo 1:16:5:10:20:4-6)

 8. Tunatangaza kuwa ule ufalme wa Yahweh utaandaliwa hapa duniani Yahshua Masihi atakaporejea mara ya pili (Matayo 6:10, Ufunuo 11:15). Hii ni kufuatilia kile kipindi cha miaka mitatu unusu cha dhiki kuu (Matayo 24:29-31). Utawala wa Yahweh utatokana na sheria yake (Matayo 6:33, IsaYa 2:1-4, Mika 4:1-5). Ujumbe wa huo utawala wa Yahweh ujao ulihubiriwa na Yahshua katika uhudumu wake wote (Marko 1:14-15, Matendo 1:6-8). Mwanzoni mwa huo utawala, wateule watatawala pamoja na Yahshua katika kipindi cha miaka elfu moja (Ufunuo 20:6 na Ufunuo 5:10). Wakati huo, wote walio epuka ile dhiki kuu watatawaliwa na Masihi na wateule wake (Danieli 7:27). Mfalme wa amani atatawala ulimwengu wote na hata wanyama watabadilishwa ili hata mbwa mwitu na mwana kondoo watakula pamoja (IsaYa 11 na Isaya 65:24-25) Yerusalem ndiyo utakuwa mji mkuu wa utawala na kuabudu katika Hekaru kutalejerewa. (Isa 2:1-4, Ezekieli 40:44) Baadaye kutakuwa na mbingu mpya na nchi mpya (IsaYa 66:22). Ni wakati huu Yerusalem mpya itashuka kutoka juu iwe duniani na Yahweh mwenyewe atakuwa pamoja na watu wake (Ufunuo 21 na 22).

 9. Tunatangaza zile Iddi takatifu (Sikukuu) katika Mambo Ya Walawi 23 na Hesabu 28 na 29 ni za kuzingatiwa kama mikutano teule. Ushahidi kote katika agano jipya waonyesha Masihi mwenyewe na hata kusanyiko la mitume waliadhimisha hizi siku teule (Luka 4:16, Matendo 17:2, Luka 22:13-15, Yohana 7:2, 10:14, 14:37, Matendo 2:1, Matendo 20:5-7, I Wakorintho 5:8). Hizi siku teule zilitabiriwa kama zitatunzwa katika ufalme wa Yahweh (Zekaria 14:16, IsaYa 66:22-24, Ezekieli 46:1). Katika unabii siku hizi ni kivuli cha mambo yajayo (Wakolosai 2:16-17)

 10. Tunatangaza Sabatu (kutoka Ijumaa jioni mpaka Sabato jioni) inafaa kutunzwa kama ya mkutano takatifu na wote wenye kuabudu na kweli. (Kutoka 20:8-11, Kumbukumbu la Torati 5:12-15, Marko 2:27-28, Waebrania 4:8-11) Sabato ni ishara dhabiti kati ya Yahweh na walio wake (Kutoka 31:12-17). Utakatifu wa sabato lazima usikiukwe (NehemiYah 13:15-22, IsaYa 56:1-8, IsaYa 58:13-14). Pamoja na hiyo sabato ya kila Juma pia twafahamu kuna ule mwaka wa kuachilia Mashanba yetu (mwaka wa sabato) na mwaka wa jubilee pia ya kuzingatiwa (Kutoka 23:10-12, Mambo ya Walawi 25:Kumbukumbu 15:) Unabii pia watabiri nyakati hizi za miaka pia ni za kuzingatiwa kama sheria ingine ile. Yahshua atazitimiza kwa kuleta ukombozi kwa wateule wake wote atakarojea ulimwengu huu (Luka 4:14-21, IsaYa 61:1-3)

 11. Tunatangaza mwandamo wa mwezi unapoonekana ndipo mwezi uanzapo, na tunao wajibu wa kuangalia huu mwandamo (Hesabu 10:10, Zaburi 81:3). Baada ya kuonekana huu mwandamo, mwezi wa maandishi takatifu huwa umeanza. Siku naye huanza na huisha jua linalotua. (Mwanzo 1:5, 8, 13, 19, 23, 31; Mambo ya Walawii 23:32). Ili tuutangaze mwanzo wa mwezi mpya lazima mwandamo uonekane na mashahidi angalao wawili wakuaminika. Mwandamo wa mwezi ndio unaamua Nyakati zilizotengwa za Yahweh yaani iddi (sikukuu). Mwezi wa kwanza katika maandishi utalingana na wakati shairi iko na mashuke (Abib) katika nchi ya Israeli (Kutoka 9:31 na 12:2 Kumbukumbu 16:1, 16). Huu mwandamo wa mwezi utazingatiwa hata katika ule ufalme wa Yahweh (IsaYa 66:23)

 12. Tunatangaza Pasaka ndiyo adhimisho la kufa na kufufuka kwa mwokozi wetu Yahshua Masihi, aliye Mwana Kondoo wa Yahweh anayetwaa dhambi zetu walimwengu (Yohana 1:29, 36). Kama alivyoweka mwokozi wetu, tunawatawadha wenzetu miguu kabla ya Ibada ya Pasaka (Yohana 13). Hii Pasaka ni jambo linalokumbukwa mara moja kwa mwaka, Tarehe 14 mwezi wa Abib, jioni baada ya jua kutua (Hesabu 28:16, 1 Akorintho 5:7-8 na 11:23, Kumbukumbu 16:6). Ni wakati kama huu Pasaka ile ya kwanza iliyo andaliwa na Yahweh kwa wana wa Israel katika nchi ya Misri (Kutoka 12:3-14). Ishara ya mwili wa Masihi katika dhabihu hii ni Mkate Usiotiwa Chachu (matzah; 1 Akorintho 5:7). Naye Damu ya Yahshua inasimamiwa na Divai Mpya isiyochachuka (Kiiberania-tirosh ama “asis”, Kumbukumbu 32:14, IsaYa 65:8-9, Matayo 26:27-29). Katika kula ule Mkate na kunywa ile Divai, tunafanya upya agano letu na Yahweh muumba wetu katika dhabihu la mwanae Yahshua aliye mkombozi wetu. Wanaoshiriki katika Pasaka kuila ni wale wamepaswa tohara kiroho katika nyoyo zao, kwa kufanya agano na Yahweh kwa kubatizwa katika Jina la Yahshua (Kutoka 12:43-48, Wakolosai 2:11-14). Siku ya Pasaka pia huwa ni ya maandalio ya zile siku za mkate usiotiwa chachu ambazo siku ya kwanza ni Sikukuu (Marko 15:42, Luka 23:54, Yohana 19:14, 31, 42) Hii ndiyo siku ambayo chachu yote huondolewa katika makazi yetu (Kutoka 12:15, Kumbukumbu 16:4) Hakuna mkate ulio na chachu huliwa siku ya Pasaka (Kumbukumbu 16:2-3) Siku Ya Pasaka yenyewe sio sikukuu. Ikiwa mtu amejitia najisi ama yuko safarini Yahweh aliwaandalia siku ingine , tarehe 14 mwezi wa pili waile pasaka (Hesabu 9:1-14)

 13. Tunatangaza baada ya pasaka kunazo zile siku za mkate usiotiwa chachu kutoka tarehe 15 hadi 21 mwezi wa Abib. Hii siku ya 21 pia ni pamoja na hizi siku (Mambo ya Walawi 23:5-8, Hesabu 28:18-18, 25). Ni wakati wa kula mkate usio na chachu siku saba na hakuna kilicho na chachu wala chachu yenyewe itakuwa katika makazi yetu (Kutoka 13:6-7, Mambo ya Walawi 23:6, Kumbukumbu 16:3-4). Chachu husimamia uovu na ubaya na kutokuwa na chachu kwashiria weupe na moyo wa kweli (1 wakorintho 5:8). Kiroho, inatufaa kuondoa mambo yote yenye kutudhuru, kama mafundisho ya uongo, dhambi na husuda (1 Wakorintho 5:6-8; Matayo 16:6, 12; Marko 8:15; Luka 12:1-3)Siku ya kwanza naya saba ya siku hizi huwa ni sabato (sikukuu) na tunamfanyia Yahweh ibada za kusanyiko takatifu (Kutoka 12:15-20, Hesabu 28:17-25). Jioni ya ile Sabatu ya Wiki iliyo katikati ya hizi siku kuu, tunamkumbuka Yahshua kama ule mganda wa malimbuko ya mavuno yetu wa kutikishwa mbele ya Yahweh (Mambo ya Walawi 23:9-11). Yahshua Masihi ndiye Limbuko letu la kwanza (1st fruits) (1 Wakorintho 15:20-22, Ufunuo 1:5). Alifufuka katika siku ya sabato katika wakati wa mkate usiotiwa chachu ili awe limbuko letu la mavuno ya kwanza la kiroho kwa Yahweh na akajipeana kwake siku ya kwanza ya juma (Matayo 28:1-2 Yohana 20 15-17) Hii ni mojawapo ya nyakati tatu watu wameagizwa kuondoka kumfanyia Yahweh sikukuu (Kutoka 23:14-17, Kumbukumbu 16:16)

 14. Tunatangaza sikukuu ya Majuma (Pentekoste) ni ya kutunzwa siku hamsini baada ya Sabato iliyo katikati ya siku za mikate isiyotiwa chachu. Limbuko letu lilitikishwa mbele ya Yahweh wakati Yahshua alifufuka baada ya ile sabato ya juma (Matayo 28:1-2). Yeye ndiye dhabihu (omer) ile ya limbuko (Yohana 20:15-17). Dhabihu hii ilikuwa yafanyiwa na kuhani katika ile siku nyumaye ya sabato ya wiki (Jua likitua sabato hadi jua likitua jumapili) katika ile sabato ya wiki iliyo katikati mwa siku za mkate usiotiwa chachu (Mambo ya Lawi 23:10-11, 15:16) Kupata siku ya pentecote ama sikukuu ya majuma twahesabu sabato saba na kuongeza siku moja kupata siku hamsini. Pentecoste huwa siku ya jumapili kila wakati,(Sabato jua likitua hadi jumapili jua likitua). Endapo Pasaka ingelifikia siku ya sabato ya juma ilikuwa desturi ya kuhani mkuu kuendesha dhabihu hii siku iliyofuatia (siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu) na hapo siku ya pentecoste ingeanza kuhesabiwa (Yoshua 5:10-12). Kimila, wayahudi hutabua siku hii kama waliyofanya upya agano na Yahweh katika mlima Sinai (Kutoka 24:1-8). Katika hii hii siku ya Pentecoste ama siku kuu ya majuma Yahweh aliwamwagia waumini wa lile shirika la mitume Roho Mtakatifu walipokuwa wamekusanyika nyumba ya juu kufuatia agizo la mwokozi wetu (Matendo 1:1-11, Matendo 2) Hii ni ya pili ya zile nyakati tatu za kuondoka kumfanyia Yahweh Sikukuu. (Kutoka 23:14-17, Kumbukumbu 16:16)

 15. Tunatangaza Sikukuu ya kuzipiga baragumu ni ya kuadhimishwa siku ya kwanza ya mwezi wa saba wa maandishi (MamboYa Walawii 23; 23-25). Hii ni sabato, siku iliyo kuu, na kutakuwa na mkutano takatifu pamoja na kupiga baragumu (Mambo ya Lawi 23:24, Hesabu 29:1). Kupiga baragumu ama tarubeta maana yake ni kutahadharisha watu (Hesabu 10:1-10, IsaYa 58:1). Katika unabii, jambo hili laangazia kuja kwa mwokozi wetu mara ya pili, Yahshua Masihi (Matayo 24:31, 1 Wakorintho 15:51-57, 1 Wathesalonike 4:16-17, Ufunuo 11:15-18)

 16. Tunatangaza Siku ya upatanisho (Yom Kippur) ni ya kuadhimishwa siku ya kumi ya mwezi wa saba wa maandishi takatifu na ni siku ya kufunga kula na kunywa kabisa (Mambo ya Lawi 23:26-32, Zaburi 35:12, IsaYa 58:3-5). Katika hii siku iliyo takatifu sana, tunakumbuka dhabihu kuu ya kufa kwa Yahshua Masihi (Mambo ya Walawi 16 na Hesabu 29:7-11). Hatuli siku hii tukitazamia katika unabii chakula cha jioni cha arusi ya mwana kondoo tutakaposherehekea na mwokozi wetu atakaporejea (Matayo 26:29, Ufunuo 19:6-9)

 17. Tunatangaza Iddi ya vibanda pia ni ya kutunzwa kutoka tarehe 15 hadi 21 mwezi wa saba wamaandishi takatifu (Mambo ya Walawii 23:33-34, 39-41) Siku ya mwanzo ya siku hizi ni sabato na kutakuwa na mkutano mtakatifu (Mambo Ya Walawii 23:35, Hesabu 29:12). Wakati huu twakumbuka jinsi Waisraeli walipokaa katika vibanda (hema) walipokuwa jangwani (Mambo Ya Walawii 23:42-43) Inatazamia ufalme wa Yahweh tunaoutarajia karibuni (Zekaria 14:16-21) na tunasherehekea tukiwa na furaha, amani na upendo wa Yahweh na watu wake. Siku ya kumalizia iddi hii, ambayo ni siku ya nane, ni Sikukuu (Yohana 7:37-39, Mambo Ya Walawii 23:36. Hii siku ni sabato kuu ambayo kuna mkutano mtakatifu (Mambo ya Walawii 23:37-38, Hesabu 29:35-38). Siku hii yatabiria wakati wa mbingu mpya na nchi mpya Yahweh atakazozifanya, wakati ambapo hekaru Yake itakuwa pamoja na watu wake, na maji ya uhai ya roho Mtakatifu yatatoshelezwa kwa wale walio na kiu (Ufunuo 21:1-7, Ufunuo 22:1-22, Yohana 7:37-39). Iddi ya vibanda ndiyo ya tatu katika zile kusanyiko za kuondoka (Kutoka 23:14-17, Kumbukumbu 16:16)

 18. Tunatangaza zile sheria za wanyama wasio liwa bado unatekelezwa (Mambo ya Walawii 11, Kumbukumbu la Torati 14. ) Ni zile tu nyama ambazo Yahweh ameidhinisha za kutumiwa katika Neno lake, zinafaa kuliwa (1 Timotheo 4:1-4, Matendo 10:14 , Matendo 11:7-8) Haifai tuchukulie vibaya sheria hii ya nyama zisizoliwa kumtenga mtu yeyote (Matendo 10:28, Matendo 10:34-35, Matendo 11:12, 17-18). Sheria hizi za kuwa najisi ni za kufundishwa na kufuatwa ili kutambua kati ya kilicho najisi na kilicho safi (Ezekieli 22:26, Ezekieli 44:23 Mambo ya Walawii 11-15). Hizi sheria hutufundisha kuwa teule na takatifu mbele za Yahweh (Mambo Ya Walawii 11:43-47 Kumbukumbu 14:2, Matayo 5:48). Yahweh apenda tuzingatie mambo haya kiroho ili tuwe tofauti na tujitenge na matendo yaliyo maovu (2 Wakorintho 6:14-18).

 19. Tunatangaza kutoa fungu la kumi ni amri iliyo muhimu ili kondoo wa malisho ya Yahweh wakalishwe na pia habari njema ikaenezwe kwa wengine ambao haijawafikia (Yohana 21:15-17, Matayo 28:19-20, 2 Wakorintho 11:7-9). Hili ni asilimia kumi ya vyote Yahweh amekuongezea (Gross income) na ni teule kwake (Mambo Ya Walawii 27:30-33). Fungu la kumi lafaa kutolewa la mshara, mapato na hata mafuno (2 Mambo Ya Nyakati 31:2-12, Matayo 23:23). Fungu la kumi linatolewa kwa Uongozi wa Shirika (Organisational treasury) na ndipo mahitaji ya kuendelesha kazi ya Yahweh yatatolewa (Malachi 3:7-12). Yampasa kila mtu akaliweke fungu lingine la pili la kumi ya kugaramia sadaka na mahitaji ya Sikukuu (Iddi) za Yahweh (Kumbukumbu 14:22-27). Kila muda wa miaka mitatu, katika mwaka wa tatu na wa sita wa msururu wa miaka saba (Sabbatical year), yampasa kila mmoja kuweka fungu lingine ya kusaidia kifedha wote walio na mahitaji (Kumbukumbu 14:28-29, Kumbukumbu 26:12-15)

 20. Tunatangaza Yahweh amepeana karama mbali mbali za kiroho katika kusanyiko la waumini ili zikaunufaishe mwili wote (1 Wakorintho 12:1-11). Kati ya hizo karama ni ile ya uponyaji. (1 Wakorintho 12:9). Wanaohitaji uponyaji wameagizwa kupakwa mafuta katika jina la Yahweh huku wakiombewa na wazee. (Yakobo 5; 13-16). Ikiwa wengine wako mbali na wazee na kuna ungumu kukutana, kitambaa ambacho kimepakwa mafuta na kuombewa na wazee kitatumiwa aliyeadhirika na magojwa (Matendo 19:11-12)

 21. Tunatangaza sheria ya Musa (Torati), Manabii, na Zaburi (Maandishi ya hekima), ndizo vipengele vitatu vya maandishi matakatifu ya Agano la Kale (Luka 24:44-45). Maandishi haya ndiyo msingi hasa wa Agano Jipya na zote hunena sawa (Yakobo 1:21-25, 2 Timotheo 3:14-15, Matayo 4:4, Yohana 5:39). Kutoka Mwanzo hadi Ufunuo, haya maandishi yote yenye pumzi ya Yahweh hayatofautiani (2 Timotheo 3:16-17, Yohana 10:35) Utabiri wa neno la Yahweh umetangaza matukio ya nyakati hizi za mwisho kuanzia mwanzo (Mwanzo 3:15, Mwanzo 49:10, IsaYa 46:9-11, Ufunuo 19:10-16, Ufunuo 1:7).

UONGOZI

Tunatangaza Baba Yahweh amepeana serikali ya kuendesha mwili wa kiroho wa waumini. Serikali hii ina Yahshua kama kiongozi wake. Amepeana nyadhifa mbali mbali teule za kuongoza ambazo kwa mafundisho kamili, zitaleta nguvu na udhabiti katika ushirika (Waefeso 4:11-16). Serikali hii ni kama Waamuzi walio wekwa zamani katika Torati (Kumbukumbu la Torati 1:13-18, Kutoka 18:13-26, Kumbukumbu la Torati 16:18-20). Ni wajibu wa wazee walio teuliwa kufanya maamuzi yafaayo katika kusanyiko ili wote wandumishe kutii sheria ya agano ya Yahweh (1 wakorintho 5:1-5, Kumbukumbu 17:2-13). Waraka huu waleta msingi wa uongozi wa kuendesha agano la Yahweh katikati ya watu wake.

Wale walioteuliwa nyadhifa za Wazee wanapaswa kuwa na kutimiza mambo fulani (1 Timotheo 3:1-3, Tito 1:5-9). Wanafaa waongoze kondoo wa Yahweh kwa kuwa mifano miema, sio kwa kushurutisha watu kwa njia mbaya, bali waongoze kwa unyenyekevu na upendo (1 Peter 5:1-5). Hao wachungaji wataonyesha mapenzi na kujitolea kwa Yahweh na Yahshua kwa kulisha kondoo wa malisho yake na Ukweli wa Yahweh ( Yohana 21:15-17). Wanao wajibu wa kulinda kondoo kutokana na mashambulio ya wenye kutenda maovu (1 Wakorintho 5:9-13, Tito 1:7-11). Wanawajibika mbele za Yahweh kutenda kama alivyotenda mtume Paulo na kutangaza mafundisho yote ya Yahweh kwa watu wake (Matendo 20:26-28) Ni kazi yao kuhubiri Neno la Yahweh ili watu waelimike nalo, pia kukaripia, kukemea na hata kuonya wandugu wote kwa mafundisho sahihi (2 Timotheo 4:1-4, Tito 2:1). Endapo mzee atashindwa kutekelea kazi hiyo yake kadiri ya maandishi takatifu, aweza ondolewa. Walakini kazi hii ni ya maishani mwote.

Kamati kuu ya kuongoza (Serikali), ni Wazee walio teuliwa na hufanya kazi kama baraza (Matendo 15:2, 4, 6). Mipango ya Ushirika na pia maswali yanayolenga imani yataletwa mbele ya kamati hii ya Wazee na baada ya kujadiliana kwa kina hoja zote, uamuzi utafikiwa kwa njia ya wote kukubaliana (Matendo 15; na Matendo 16:4). Uamuzi wowote ni lazima uwe sembamba na Neno la Yahweh kama Roho Mtakatifu atakavyo pendekeza (Matendo 13-1-5;Yohana 14:15-17, 25-26;Yohana 15:26, 1 Yohana 5:7). Iwapo kuna Makusanyiko mandogo katika vijiji na visehemu, watawekewa kamati za kuwaongoza ambao watakuwa chini ya ile kamati kuu (Tito 1:5). Kuteuliwa kutafanyika kama kunahitajika na pia vile roho akiwaongoza wazee kufanya hivyo (Matendo 6:1-6, 1 Timotheo 4:14). Wenye kuteuliwa ni lazima watachunguzwa vyema na wazee (1 Timotheo 5:22). Mambo ya kifedha yataendeshwa na hizi kamati za wazee. Na ili kutimiza malengo ya kisheria “Yahweh’s Philadelphia Truth Congregation” ina nyadhifa za Mwenyekiti, Makamu, Mweka-hazina na pia Mwandishi. Nyadhifa hizi zitajazwa kila mwaka katika mkutano mkuu wa wazee katika iddi ya vibanda.

Viongozi wa kusanyiko hili imewabidi kuenenda katika njia inayo onyesha upendo na heshima kwa wandugu wote (1 Timotheo 5:1-2, 1 Peter 5:1-4). Wandugu pia imewalazimu kuwaheshimu sana na kuwatii wale walio katika nyadhifa za uongozi (1 Timotheo 5:17-20). Katika hali ya kunyenyekea imetubidi kuwatii Wazee walioteuliwa huku nao wakituongoza kwa njia ya upendo (Waebrania 13:7-17, 17:1 , 1 Peter 5:5-6). Yahshua ndiye mchungaji mwema anayelisha kondoo wake (Yohana 10:1-18, Mhubiri 12:11). Wazee wateule (Wachungaji), kama vile Yahshua, ni lazima wawe na upendo mkuu sana kwa Kondoo wa malisho ya Yahweh, upendo utakaowapelekea kuwasaka kondoo hata waliopotea (Luka 15:3-7)

Kudhihirisha upendo mkuu na heshima kati ya wandugu ndani ya shirika hili la Yahweh kutaleta ushikamano wa kifamilia. Shikamano hili la kifamilia ndilo launganisha Watu wa Yahweh na Baba Wetu wa Mbinguni na hata pia Mwanawe, Yahshua. Ndiposa upendo wa Yahweh unadhihirika katika maisha ya walio wake. “Wala sio hao tu ninaowaombea, lakini na wale watakaoamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo mmoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa wewe ndiye ulinituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi. Baba hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo. Wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; maana ulinipenda kabla ya kuweka msingi ulimwengu. (Yohana 17:20-24)

MSHIRIKI WA KUSANYIKO LA FILADELFIA NA UKWELI WA YAHWEH

Ili ukahesabiwe kuwa mshiriki katika Kusanyiko la Filadelfia na Ukweli wa Yahweh (YPTC) ni lazima mtu atimize yafuatayo.

Lazima mtu awe anakaa maisha ya toba akiwa ametubu dhabi zake zote za zamani na anatunza sheria ya agano ya Yahweh (Matendo 2:37 na 3:19) Pili lazima awe amebatizwa katika Jina la Yahshua aliye Masihi (Matendo 2:38). La tatu ni lazima awe amepata kipawa cha roho mtakatifu kwa kuwekelewa mikono na Wazee walioteuliwa (Matendo 8:17 na 19:5-6) Mwishowe awe mwenye kutii katika kushikilia ushirika huu (2 Wakorintho 9:6-15 na 11:8-9, Matayo 6:19-21) katika kulisha kondoo wa malisho ya Yahshua (Yohana 21:15-17), na kueneza habari ya Ufalme ujao hivi karibuni wa Yahweh (Matayo 28:19-20 na Matendo 1:6-8) na pia katika kutimiza zile amri mbili zilizo kuu kama alivyo zipeana mwokozi wetu Yahshua aliye Masihi (Matayo 22:36-40)

Wanaotimiza mambo haya watahesabiwa kuwa washiriki wetu walio wema.

Ni wajibu wa kila mmoja kuichukulia habari hii ya wokovu katika moyo wake na kuishi maisha yanayolingana na sheria na agano la Yahweh. ”Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii siku zote, si wakati nilpokuwapo tu, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Yahweh atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake njema” (Wafilipi 2:12-13)

Ukitaka ukweli zaidi wa Biblia unaweza kutupata kwa tovuti

www.yahstruth.org

Ama tuandikie barua kupitia anwani ifuatayo

Yahweh’s Philadelphia Truth Congregation
S.L.P 547
Loganville, GA. 30052

Ukiwa Africa utaandikia
Peter N Warari
Yahweh’s Philadelphia Truth Congregation
S.L.P. 3496 00200 Nairobi

Barua Pepe: nwarari@hotmail.com
Ama: wararin@yahstruth.org
Simu: 020 813004
Simu ya Mkono: 0722 271520